TANZIA :: AMNYONGA MJOMBA WAKE KISA KUMFUKUZA NYUMBANI KWAKE
Mkazi wa Kijiji cha Mwai, Kata ya Mtenga wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, Said Matenga (50), ameuawa kwa kunyongwa kwa kamba na mpwa wake baada ya kumfukuza nyumbani kwake kutokana na tabia za wizi.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku katika kijiji hicho, wakati marehemu akitoka kunywa pombe katika kilabu kilichopo kijijini hapo.
Alisema siku moja kabla ya tukio hilo, Matenga alimfukuza nyumbani kwake mpwa wake huyo aitwaye Singu George (35) kutokana na tuhuma za kuiba vitu vya nyumbani kwake na kwenda kuviuza ili apate fedha ya kununulia pombe.
Baada ya mpwa wake huyo kufukuzwa nyumbani kwa babu yake, kitendo hicho kilimkasirisha na kuwahusisha rafiki zake waliofahamika kwa majina ya Mathias Said (28) pamoja na Luleka Luhende (28) ambao walimvizia mzee Matenga na kisha kumuua kwa kumnyonga na kamba shingoni.
Kamanda Kyando alisema baada ya watuhumiwa hao kufanya mauaji hayo waliutupa mwili wa marehemu kwenye majani karibu na Mto Lita uliopo kijijini hapo.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya uchunguzi zaidi na watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika, ili wakajibu tuhuma zinazowakabili.
source mtanzania
No comments: